Na: mwandishi wetu.
Maonesho
ya ukakamavu na mbinu za medani katika kupambana na adui hasa kulinda
amani ya nchi yetu kutoka Kikosi Maalum cha Makomandoo wa Jeshi la
Wananchi Tanzania (JWTZ), itakuwa ni sehemu ya shamrasha zitakazopamba
maadhimisho ya miaka 53 ya Muungano yatakayofanyika kwa mara ya kwanza
mjini Dodoma Aprili 26 mwaka huu.
Kwa
mujibu wa taarifa iliyotolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu
Sera, Bunge, Ajira, Kazi, Vijana na Watu Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama
maadhimisho hayo yanatarajiwa kuhudhuriwa na Rais Dkt. John Pombe
Magufuli, pia yatapambwa na burudani nyingine kutoka vikundi mbalimbali.
Taarifa
ya Waziri Mhagama ametaja shughuli nyingine zinazotarajiwa kufanyika
siku ya Muungano kuwa ni gwaride la heshima lililoandaliwa na vikosi vya
ulinzi na usalama (JWTZ,JKT, Polisi na Magereza) na onesho la mbwa na
farasi waliofunzwa.
Aidha,
Waziri Mhagama aliongeza kuwa mambo mengine yatakayofanyika ni gwaride
la uzalendo la wanafunzi wa shule za sekondari za Dodoma, burudani za
vikundi vya ngoma za asili kutoka Dodoma na Zanzibar, Yamoto Band,
vikundi vya muziki wa kizazi kipya kutoka kwa wasanii Mchungaji Zayumba,
Jacob Beats, Mwenge Jazz Band na Mgosi Maturumbeta.
“Kauli
mbiu ya sherehe za kutimiza miaka 53 ya Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar ni Miaka 53 ya Muungano; Tuulinde na Kuumarisha, Tupige Vita
Dawa za Kulevya na Kufanya Kazi kwa Bidii,” alifafanua Waziri Jenista Mhagama.
Ametoa
wito kwa wananchi wote nchini kusherehekea siku hiyo muhimu kwa
kudumisha amani, upendo, umoja na mshikamano kwa maendeleo ya nchi.
“Ninaomba
kuchukua nafasi ya pekee kuwaomba wananchi wote waliopo Dodoma
kujitokeza kwa wingi uwanja wa Jamhuri siku hiyo ya Jumatano tarehe 26
Aprili 2017 kuanzia saa 12:00 asubuhi ili kusherehekea kwa pamoja
maadhimisho hayo muhimu kwa nchi yetu,” alisema Jenista Mhagama.
Maadhimisho
ya Muungano yanafanyika kwa mara ya kwanza Dodoma ikiwa ni siku kadhaa
tangu Serikali ya Awamu ya Tano ianze kutumiza azma ya kuhamia katika
makao makuu hayo mapya
JAMII VIEWER
0 comments:
Post a Comment