Saturday, 18 June 2016

Yanga yashusha jangwani bonge lamchezaji kwa 240milioni

Leave a Comment


YANGA imemnasa mshambuliaji mpya raia wa Zambia, Obrey Chirwa anayechezea klabu ya Platinum FC ya Zimbabwe kwa kitita cha dola za Marekani 120,000 (zaidi ya Sh milioni 240 za Tanzania).
Kwa mujibu wa gazeti la The Herald la Zimbabwe jana lilieleza kuwa Chirwa ambaye amewahi kuichezea timu ya Konkola Blades ya Zambia, ameifungia Platinum mabao matano katika mechi nane alizocheza kwenye Ligi Kuu ya Zimbabwe.
Chirwa, ambaye yumo kwenye kikosi cha timu ya taifa ya vijana ya Zambia chini ya umri wa miaka 23 imeelezwa na gazeti hilo kuwa aliondoka Zimbabwe juzi kuja Dar es Salaam na alitarajiwa kuwasili Dar es Salaam jana.
Chirwa anatarajia kushirikiana na mshambuliaji mahiri wa Yanga Donald Ngoma, ambaye pia ametokea timu hiyo ya Zimbabwe. Awali Yanga ilikuwa ikimuwania winga Walter Musona kutoka Platinum kabla ya kughairi dakika za mwisho na Chirwa kuonekana mtu sahihi kwa nafasi hiyo.
Viongozi wa Yanga hawakupatikana jana kuzungumzia suala hilo na hata Kocha Mkuu wa timu hiyo, Hans Pluijm ambaye yupo Algeria na Yanga, alipotafutwa kwa njia ya mtandao kuhusu usajili huo alisema hana cha kuzungumza.
Wakati huohuo, Yanga iliwasili salama jana asubuhi nchini Algeria tayari kwa mchezo wa Kundi A Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF CC) dhidi ya wenyeji MO Bejaia. Nahodha wa timu hiyo Nadir Haroub ‘Cannavaro’ alisema wachezaji wote wapo katika ari ya ushindi kwa ajili ya mchezo huo utakaofanyika Uwanja wa Unite Maghrebine mjini Bejaia, Algeria.
“Nashukuru tumewasili salama hapa Bajaia, wachezaji wote tupo salama hakuna majeruhi na kila mmoja wetu ana ari kuhakikisha tunaanza vizuri kwa kupata ushindi ili kujiweka kwenye mazingira mazuri ya ushindi,”alisema Cannavaro.
Yanga iliingia kwenye hatua ya makundi ya mashindano hayo kwa mara ya kwanza kwenye historia ya klabu hiyo baada ya kuitoa Sagrada Esperanca ya Angola kwa mabao 2-1, ikiwa ni baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 nyuma kabla ya kufungwa 1-0.
Mechi hiyo itachezeshwa na waamuzi wa Morocco, Bouchaib El Ahrach atakayekuwa katikati akisaidiwa na Redouane Achik na Youssef Mabrouk. Baada ya mchezo huo, Yanga itarejea Dar es Salaam kuwakaribisha mabingwa wa Afrika, TP Mazembe Juni 28.
                                                                                            JAMII VIEWER
If You Enjoyed This, Take 5 Seconds To Share It

0 comments: