Tuesday, 7 June 2016

wanne wasajiliwa na yanga mmoja atokea msimbazi

Leave a Comment



Na mwandishi wetu

KIPA wa timu ya Prisons ya Mbeya, Benno Kakolanya, amemalizana na klabu ya soka ya Yanga baada ya kusaini mkataba mnono wa miaka miwili kuichezea timu hiyo uliogharimu shilingi milioni 35.

Usajili wa Kakolanya ulifanyika sambamba na beki mahiri wa timu ya Mtibwa Sugar, Vicent Andrew, aliyejiunga na timu hiyo ya mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kakolanya anatarajia kunyakua mshahara wa shilingi milioni 1 kwa mwezi, usajili huo utakuwa ukikamilisha idadi ya wachezaji wanne waliosajiliwa katika klabu hiyo baada ya Juma Mahadhi aliyekuwa timu ya Coastal Union na Hassan Kessy aliyekuwa akicheza timu ya Simba.
Baada ya usajili huo, Yanga sasa itakuwa na makipa wanne ambao ni Ally Mustapha ‘Barthez’, Deogratius Munishi ‘Dida’, Benedicto Tinoco na Kakolanya, lakini inadaiwa kuwepo uwezekano mkubwa wa kipa mkongwe ‘Barthez’ kupewa mkono wa kwaheri.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Kakolanya alisema kutua Yanga ni hatua kubwa katika maisha yake ya soka kutokana na ubora wa timu hiyo, akiongeza kuwa yupo tayari kupambana ili kucheza kikosi cha kwanza katika timu hiyo.

“Sikufikiria kama siku moja nitakuwa sehemu ya kikosi cha Yanga, lakini nashukuru Mungu kwa hatua hii niliyofikia najua changamoto iliyopo mbele yangu.
“Nitahakikisha nakuwa bora kila siku ili niweze kuendana na kasi ya ushindani wa namba iliyopo katika timu hiyo, hata hivyo hali hiyo hainiogopeshi kutokana na uwezo nilionao,” alisema Kakolanya.

Mafanikio ya Kakolanya yalionekana muda mfupi baada ya kuonesha uwezo mkubwa msimu huu, akicheza michezo 19 ya Ligi Kuu Tanzania Bara na kufungwa mabao manane tu huku akiisaidia Prisons kumaliza katika nafasi ya nne mbele ya Mtibwa iliyomaliza ikiwa nafasi ya tano.
If You Enjoyed This, Take 5 Seconds To Share It

0 comments: