Tuesday, 14 June 2016

ITALIA yataka kuidhamini Yanga

Leave a Comment


NA MWANDISHI WETU

KAMPUNI ya Macron S.p.A. ya vifaa vya michezo nchini Italia inataka kuingia Mkataba wa udhamini wa vifaa vya michezo na klabu ya Yanga ya Dar es Salaam.
Na sasa kampuni hiyo yenye maskani yake mjini Crespellano, Bologna inahaha kuhakikisha Yanga inatumia jezi zenye nembo yake katika mchezo wa kwanza wa Kundi A Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya wenyeji Mouloudia Olympique Bejaia Jumapili Algeria.


Kampuni hiyo inayosifika kama inaongoza kwa vifaa bora vya michezo Ulaya, imekabidhi Yanga seti mbili za jezi za nyumbani na ugenini, kwa ajili ya Kombe la Shirikisho pamoja na nguo za kuvaa wakati wa mapumziko na safarini.

Yanga walivaa jezi za Macron wakati wanakwenda Uturuki Jumapili kuweka kambi ya kujiandaa na mchezo wa Jumapili, lakini hawatavaa jezi za kampuni hiyo katika mchezo na MO Bejaia kwa sababu hawajaziandikisha Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Yanga itavaa jezi zilizotolewa na CAF ambazo watabandika nembo ya mdhamini wao mkuu, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) sambamba na nembo ya mdhamini wa mashindano.
Katika hatua nyingine, uongozi wa Yanga tangu wiki iliyopita unahaha kupata fedha za ushindi wa Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation Cup (ASFC) bila mafanikio.


“Sasa hatujui kama ni Azam ndiyo hawajakabidhi hizo fedha TFF, au ni TFF wamekabidhiwa lakini hawataki kutupa. Mashindano yamekwisha, sisi ndiyo mabingwa, tupewe chetu,”kimesema chanzo.

Yanga pia inahangaikia fedha za ubingwa wa LIgi Kuu ambazo wanapaswa kupewa na wadhamini wao, TBL kwa mujibu wa Mkataba.
Katika Mkataba wa udhamini wao, TBL imeweka kipengele cha kuipa zawadi Yanga ikitwaa ubingwa au nafasi ya pili katika Ligi Kuu – hata hivyo hadi sasa hawajapatiwa zawadi hiyo.   
Yanga imeweka kambi katika hoteli ya Rui mjini Antalya, Uturuki tangu Jumapili na itaondoka Ijumaa kuingia Bejaia, Algeria tayari kwa mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu.

                                                                                                            JAMII VIEWER

If You Enjoyed This, Take 5 Seconds To Share It

0 comments: