Tuesday, 14 June 2016

Lowassa Awaandikia Jeshi la polisi barua ya angalizo

Leave a Comment


Waziri Mkuu wa Zamani, Edward Lowassa ambaye pia alikuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema akiungwa mkono na vyama vya upinzani vinavyounda Ukawa, jana alimuandikia waraka Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu.

Waraka huo ulijikita katika maagizo ya Jeshi hilo kupiga marufuku mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa pamoja na kuwashikilia na kuwahoji viongozi wa vyama hivyo akiwemo mwenyekiti wake, Freeman Mbowe hivi karibuni.

Lowassa alimueleza IGP kuwa amelazimika kumuandikia barua hiyo ili kuweka kumbukumbu sahihi baada ya kupata taarifa za kuzuiwa kwa viongozi wa Chadema kufanya mikutano wakati yeye alipokuwa nje ya nchi.

Alihoji sababu za kiintelijensia zinazotolewa na jeshi hilo kuzuia mikutano hiyo kwa madai kuwa limebaini kuna uwezekano wa kutokea vurugu zimetumika ili kuhalalisha uminywaji wa demokrasia ya vyama vya siasa kwani hata historia inaonesha vinginevyo.

“Uzoefu wa historia unakinzana na madai hayo, kwa sababu yako matukio mengi ambayo yamethibitisha kwamba mijumuiko ya wanasiasa wa vyama vya upinzani, yakiwemo maandamano na hata mikutano ya hadhara yamefanyika kwa amani,” alisema.

“Iko mifano mingi inayoonesha kwamba tumefanya shughuli mbalimbali za siasa kwa maana ya maandamano na mikutano ya hadhara kwa amani na pasipo kuwapo hata ulinzi wa polisi,” alisema Lowassa kwenye waraka huo.

Alisema kuwa sababu hizo ndizo zinazopelekea wao kupinga maagizo hayo ya polisi ya kuzuia kufanyika kwa mikutano kwa kuwa sababu za kiintelijensi zinatumika kama kichaka cha misukumo iliyo nyuma ya maagizo hayo.
                                                                                                     JAMII VIEWER
If You Enjoyed This, Take 5 Seconds To Share It

0 comments: