Wakati timu yake ikiwa kambini nchini Uturuki, Kocha Mkuu wa Yanga Mholanzi, Hans van Der Pluijm amesisitiza umakini kwa wachezaji wake wote ili wasije wakafanya makosa ndani ya uwanja na baadaye yakawagharimu.
Kauli hiyo, ameitoa kocha huyo ikiwa siku mbili kabla ya mechi ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika kati ya timu yake na MO Bejaia ya Algeria, mchezo utakaopigwa keshokutwa Jumapili.
Yanga ipo nchini Uturuki tangu Jumapili iliyopita ikiwa na nyota wake wapya, Hassan Kessy, Juma Mahadhi, Vincent Andrew ‘Dante’ na Beno Kakolanya kwa ajili ya kambi ya mchezo huo.
Pluijm alisema soka ni mchezo wa makosa, lakini hataki litokee hilo kwa hofu ya kuwapa nafasi wapinzani wao.
Pluijm alisema, bado anaendelea kukiimarisha kikosi chake kwa kuwapa mbinu, ufundi na kucheza soka la haraka kitimu ili wapate pointi tatu ugenini.
Aliongeza kuwa, juzi Jumatano wachezaji na benchi la ufundi waliiangalia video ya wapinzani wao MO Bejaia na kugundua sehemu zenye madhara na kugawa majukumu kwa kila mchezaji kuhakikisha wanaibuka na ushindi Algeria.
“Sitaki kuwapa presha wachezaji kwenye mechi na MO Bejaia, ninachotaka kuona wachezaji wangu wanacheza kitimu bila ya hofu yoyote ili turejee nyumbani na pointi muhimu.
“Hatutaki kufanya makosa kwenye mechi yetu hii kwa hofu ya kuwapa nafasi wapinzani wetu kutumia makosa yetu kutufunga, hivyo tutacheza kwa tahadhari kubwa kwenye mechi hiyo, licha ya soka kuwa ni mchezo wa makosa.
“Ninaamini kama wachezaji wangu wakicheza kwa nidhamu kwa kuzingatia maagizo yake, basi tunawafunga MO Bejaia, pia umoja na dua za Watanzania zinahitajika kutusaidia kupata ushindi,” alisema Pluijm.
Mechi hii inatarajiwa kupigwa Jumapili kuanzia saa sita usiku kwa saa za Afrika Mashariki na inasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka hapa nchini.
JAMII VIEWER
0 comments:
Post a Comment